HAI
Jumla ya vikundi
11 vya kina mama na vijana
wilayani Hai mkoani Kilimanjaro vimepokea hundi ya mikopo ya jumla ya shilingi
milioni 30 kutoka kwenye asilimia kumi ya mapato ya halmashauri kama
inavyoelekezwa na serikali.
Akikabidhi hundi hizo kwa vikundi hivyo mwenyekiti
wa halmashauri ya wilaya ya Hai Bi. Helga Mchomvu amewataka wanufaika wa mikopo
hiyo kuzitumia pesa hizo ipasavyo kwa miradi ya uzalishaji ili waeweze
kurejesha fedha hizo ili wakina mama wengine na vijana waweze kunufaika.
Amesema kuwa baadhi ya vikundi vinashindwa kufikia
malengo ya kukua kiuchumi kutokana na baadhi yao kuelekeza fedha hizo katika
matumizi binafsi yasiyokuwa ya uzalishaji ikiwa ni pamoja na baadhi yao
kufanyia anasa jambo ambalo linakwamisha mpango wa utoaji huo kufikia malengo
yake.
Mchomvu ameongeza kuwa madiwani wanaotoka katika
kata za vikundi vilivyopokea mikopo hiyo kuhakikisha wanafuatilia kwa
ukaribu mienendo ya miradi hiyo na kuhakikisha matumizi sahihi yanafanywa kama
ilivyokusudiwa.
Kwa upande wake Husna Thomas ambaye ni mwenyekiti wa kikundi cha Amani
kilichopo kijiji cha Chekimaji kata ya
Masama Rundugai wanaojishughulisha na uuzaji wa mpunga na maharage ameishukuru
serikali kwa kutenga asilimia hizo kwa wanawake na vijana jambo ambalo
litawasaidia kutatua changamoto za kiuchumi.
Naye Mohamed Yusuph ambaye ni mwenyekiti wa kikundi
cha mbalamwezi katika kata ya Bomang’ombe ameahidi kusimamia fedha hizo katika
kikundi ili ziweze kutumika ipasavyo kwenye miradi mbalimbali ya kimaendeleo na
kujikwamua kiuchumi.
Awamu inayo kuja Baraza la Madiwani la halmashauri
hiyo limekusudia kutenga asilimia mbili toka katika asilimia kumi na
kuzielekeza kwa watu wa makundi maalumu hasa walemavu ili nao waweze kunufaika
na mikopo hiyo kutatua changamoto zinazo wakabili.
No comments:
Post a Comment