Saturday, 21 April 2018

DC HAI AAGIZA MTO KUFANYIWA USAFI BAADA YA MAFURIKO KUTOKEA



Meneja wa TARURA Wilaya ya Hai Mhandisi Charles Marwa (kulia) akitoa maelezo katika kijiji cha sanya station katika kata ya Kia baada yakukumbwa na mafuriko.

Mkuu wa wilaya ya Hai Mh. Onesmo Buswelu Akitoa maelekezo kwa viongozi wa kijiji cha sanya station, pamoja na maafisa mazingira wilaya mara baada ya kijiji hicho kukumbwa na mafuriko.

Mkazi wa kijiji cha sanya station akizungumzia athari ziliz
otokea mara baada ya mafuriko kutokea kijijini hapo.




Eneo ambalo mto umeacha njia yake rasmi nakutengeneza mto mwingine pembeni mara baada ya mvua kubwa kunyesha katika kijiji cha sanya station kata ya Kia wilayani Hai( Picha zote na Davis Minjer)





NA Adrian Lyapembile na Davis Minja
HAI

Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Mhe. Onesmo Buswelu amewaagiza wataalamu wa mazingira, kilimo na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kushirikiana kufanya usafi ndani ya mto Sanya eneo la Sanya Staion kuondoa mlundikano wa mchanga kwenye kina cha mto huo pamoja na kupanda miti na makingamaji kwenye eneo la mto alipofanya ziara ya kukagua madhara yaliyosababishwa mvua zinazoendelea kunyesha na kufanya mto kuacha njia ya asili na kuanzisha mkondo mwingine.

Buswelu ametoa agizo hilo hapo jana alipofika eneo la ardhi lililoharibiwa na maji ambayo yameanzisha mto mwingine unaoelekea kwenye mashamba na makazi ya wananchi wa kijiji cha Sanya Station katika kata ya Kia na kusababisha uharibufu wa mazao.

Mkuu huyo wa Wilaya pia ameliagiza jeshi la Mgambo wilaya ya Hai kushirikiana na wananchi katika kutoa nguvu kazi wakati wa zoezi la kusafisha mto huo kwa lengo la kukamilisha kazi hiyo kwa haraka ili kuzuia uharibifu mwingine unaoweza kutokea kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Pamoja na agizo hilo, Buswelu amewataka wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na mto huo kuchukua hatua za kutunza mazingira kwa kuotesha miti na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo ndani ya mita 60 kutoka eneo la mto.

Akizungumzia uharibifu uliojitokeza kwenye mazao ya wakulima, kaimu mtendaji wa kata ya Kia Simba Lema amesema zaidi ya ekari 477 zimepitiwa na maji na kwamba tathmini inaendelea kufanywa ili  kubaini gharama halisi ya madhara yaliyopatikana kwenye mazao.

Naye meneja wa TARURA wilaya ya Hai mhandisi Charles Marwa amesema kutokana na umuhimu wa mto huo kwa jamii watasimamia zoezi hilo kwa kutoa ushauri wa kitaalam na kwa haraka zaidi kama walivyoagizwa na Mkuu wa wilaya  ili kuwawezesha wananchi walioathiriwa na kuchepuka kwa mto huo kuendelea na shughuli za kijamii na kiuchumi.

No comments:

Watumiaji wa Barabara Watakiwa Kutii Sheria za Usalama

Mkuu wa Kitengo cha Usalama barabarani Mkoa wa Kilimanjaro Mrakibu Msaidizi wa Polisi Sauda Mohamed akizungumza na wananchi kwenye ...