Na Gasper Mushi
HAI
Wito umetolewa kwa wapanda pikipiki mkoa
wa Kilimanjaro kuvaa kofia ngumu (Helmet) wanapotumia vyombo hivyo vya
moto ili kujilinda na kufuata sheria za usalama barabarani.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kitengo
cha Usalama barabarani Mkoa wa Kilimanjaro Mrakibu Msaidizi wa Polisi
Sauda Mohamed wakati akizungumza na wananchi wa moka huo kupitia Redio
Boma Hai FM katika kipindi cha Siku Mpya kinachoruka kila siku saa 11
alfajiri hadi saa 3 kamili asubuhi.
Kamanda huyo wa usalama barabarani
amesema kuwa kutakuwa na oparesheni maalumu katika wilaya ya Hai ya
kuwakamata waendesha pikipiki wote wasiovaa kofia ngumu na kuwachukulia
hatua za kisheria.
Kamanda Sauda amesisitiza kuwa kila
mwendesha pikipiki anatakiwa kufuata sheria zote za usalama barabarani
kama watumiaji wengine wa vyombo vya moto na kuongeza kuwa ni makosa kwa
mwendesha pikipiki kukipita chombo kingine cha moto (kuovateki) kwa
upande wa kushoto na kwamba atakayefanya hivyo atachukuliwa hatua za
kisheria.
Kwa upande wake Mkuu wa Usalama
barabarani Wilaya ya Hai ASP Abdalah Mbaruku amesema kuwa oparesheni
hiyo itaanza wiki hii na itakuwa endelevu kuhakikisha kuwa kila mtu
anatii sheria bila shuruti kwa kuvaa kofia ngumu na kufuata sheria za
usalama barabarani kwa ajili ya usalama wa mali na maisha ya watumia
barabara wote.
Mbaruku ameongeza kuwa kosa la kushindwa
kuvaa kofia ngumu linawahusu madereva wa pikipiki pamoja na abira wao
na kwamba abiria atawajibishwa kwa kutovaa kofia na dereva
atakayeshindwa kumpatia abiria wake kofia ngumu atachukuliwa hatua kwa
mujibu wa sheria kwani kila mpanda pikipiki awe dereva au abiria anao
wajibu wa kuvaa kofia ngumu.
Aidha watumiaji wote wa barabara
wameaswa kujielimisha na kuzifahamu sheria za usalama barabarani pamoja
na kuwa waangalifu wanapotumia barabara ili kujihakikishia usalama wao
pamoja na watumiaji wengine kwa kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa
tatizo la ajali za barabarani.
No comments:
Post a Comment