Friday, 29 December 2017

SERIKALI YAOMBWA KUIMARISHA ULINZI KWA WENYE ULEMAVU WA NGOZI






Na Kija Elias, Hai.


SERIKALI imeombwa kuongeza nguvu katika kuimarisha ulinzi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), ili nawao waendelee kuyafurahia maisha ya hapa ulimwenguni.





Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Parokia ya Hai Mjini, Padri Augustino Ndepanisho, wakati wa Misa ya  maadhimisho ya Siku ya watoto Mashahidi kwenye shule ya Mt. Fransis wa Assis inayowatunza watoto wenye ulemavu wa ngozi.



Alisema kuwa serikali bado inawajibu mkubwa wa kuhakikisha inavikomesha vitendo vya ukatili vinavyoendelea hapa nchini,  dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) vya kuwauwa kwa kuwakata viungo vyao na kwamba wale wote wanaofanya vitendo hivyo, washughulikiwa kwa mujibu wa sheria.



“Leo hii katika ulimwengu wetu bado akina Herode wapo na wameongezeka,  wanaukatili mkubwa sana usioelezeka na kwamba wana roho ya ukatili,”alisema.



Naye Padri Adanthony Marunda wa Jimbo la Moshi, alisema kila Jamii inapaswa kutambua thamani ya uhai wa kila mtu, kwa kutetea maisha yao  ikiwemo kuwapatia elimu, mavazi pamoja na chakula.


Alisema wapo baadhi ya watu wamekuwa wakifanya vitendo vya ukatili kwa watu wenye ulemavu wa ngozi ili waweze kulinda ufalme wa familia zao.



Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira ambaye alifika katika shule hiyo amesema kuwa serikali ya mkoa imejipanga kuhakikisha kwamba inaweka ulinzi wa kutosha kwa watoto wenye ulemavu wa ngozi katika shule hiyo.



“Watu wenye ulemavu wa ngozi bado ni wengi katika mkoa wetu hususan katika wilaya ya Hai na Siha, hivyo serikali itaweka ulinzi wa kutosha katika shule hii ambayo inawatunza watoto hawa.

  
Awali akipokea misaada mbalimbali kutoka kwa familia ya Patrick Boyi Safi iliyofika katika shule hiyo na kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo chakula Mkuu wa shule ya msingi ya Mt. Francis wa Assis Sister Costantina, ameipongeza familia hiyo kwa kuguswa na changamoto zinazowakabili watoto hao.



Hata hivyo Sister Costantina ameiomba serikali kuwapatia askari wenye silaha watakaoweza kutoa ulinzi kwa watoto hao katika shule hiyo.

  
Akizungumza mara baada ya kutoa misaada hiyo Patrick Boyi Safi,amesema ameguswa na changamoto ya watoto hao wenye ulemavu wa ngozi na kuona kuwasaidia ili na wao waweze kujiona kwamba jamii haijawatenga.



Mwisho. 

No comments:

Watumiaji wa Barabara Watakiwa Kutii Sheria za Usalama

Mkuu wa Kitengo cha Usalama barabarani Mkoa wa Kilimanjaro Mrakibu Msaidizi wa Polisi Sauda Mohamed akizungumza na wananchi kwenye ...